Home Local General Rais Kikwete akabidhi Tuzo kwa Mama Maria Nyerere

Rais Kikwete akabidhi Tuzo kwa Mama Maria Nyerere

Rais  Jakaya Kikwete akimkabidhi Mama Maria Nyerere, tuzo la taifa la Burundi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemkabidhi Mama Maria Nyerere, tuzo la taifa la Burundi ambalo limetolewa kwa Mwalimu Julius Nyerere kuenzi mchango wake katika maendeleo ya nchi hiyo jirani.

Katika hafla hiyo fupi iliyofanyika jumatatu Julai 9 Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemwambia Mama Maria kuwa wakati wa Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi mjini Bujumbura Julai 2, mwaka huu, Rais wa nchi hiyo, Jean-Pierre Nkurunziza alitangaza kuwa taifa la Burundi lilikuwa limewatunuku tuzo mbali mbali watu mbali mbali duniani wakiwamo raia wa Burundi na wasiokuwa raia wa nchi hiyo kutokana na mchango wao katika maendeleo ya Burundi.

Rais Kikwete amesema kuwa mmoja wa watu mashuhuri duniani waliotunukiwa tuzo ni Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Yeye alitunukiwa ‘Order of the National Republic of Burundi’, Tuzo ya juu kabisa ambalo Burundi hutoa kwa watu mbali mbali kutokana na michango yao kwa maendeleo ya taifa hilo jirani.

Rais Kikwete ambaye aliiwakilisha Tanzania kwenye sherehe hizo amesema kuwa alipokea tuzo kwa niaba ya Mwalimu Julius Nyerere.

“Kwa hakika, hata sisi tulishtukizwa kwa sababu hatukujua kuwa ilikuwapo mipango ya kumtunuku Baba wa Taifa. Kama tungejua mapema ni dhahiri kuwa tungekuwezesha kwenda mwenyewe Bujumbura kupokea tuzo hiyo,” Rais amemwambia Mama Maria Nyerere.

Wakati akitangaza tuzo hiyo kwa Mwalimu, Rais Nkurunziza alimwaga sifa kwa Mwalimu na taifa la Tanzania kutokana na mchango wake katika maendeleo ya Burundi.

Rais Nkurunziza alitangaza kuwa Mwalimu anatunukiwa Tuzo hiyo kwa sababu mbili kubwa ambazo ni Kwanza, mchango wa Mwalimu Nyerere katika kuleta Uhuru wa Burundi mwaka 1962. Rais Nkurunziza alitangaza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mshauri muhimu wa kiongozi wa harakati za kudai uhuru za Burundi, Hayati Prince Loius Rwagasore aliyeuawa Oktoba 13, 1961, kabla hata Burundi haijapata uhuru.

Pili, ni mchango wa Mwalimu katika jitihada kubwa za kuleta amani katika Burundi kufuatilia vita ya wenyewe kwa wenyewe kuanzia 1995. Mwalimu alikuwa Mwezeshaji (Facilitator) wa kwanza wa mazungumzo ya amani ya Burundi na baada ya kifo chake, nafasi hiyo ilichukuliwa na Mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini ambaye naye ametunukiwa na Taifa la Burundi kwa jitihada zake.

Katika hotuba yake, Rais Nkurunziza pia aliisifu na kuishukuru Tanzania na viongozi wake wa awamu mbali mbali kwa mchango wake katika maendeleo ya Burundi ikiwa ni pamoja na kukubali kubeba mzigo wa wakimbizi wa Burundi waliozalishwa na migogoro ya kisisiasa na kiusalama katika miaka ya 1965, 1972, 1988, 1991 na 1993.

Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu Dar es Salaam.

Last Updated ( Tuesday, 10 July 2012 12:52 )  
Banner