Home Local General Mahiza apiga marufuku azuia mifugo kuingizwa Pwani

Mahiza apiga marufuku azuia mifugo kuingizwa Pwani

Mkuu wa mkoa Pwani,  Mwantum Mahiza Kufuatia kuzuka mapigano makali kati ya wafugaji na wakulima katika mji wa Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Mkuu wa mkoa huo  Mwantum Mahiza amezuia na kusitisha zoezi la uingizaji wa mifugo inayoingizwa mkoani humo na wafugaji waliohamishwa kutoka bonde la mto Ihefu  na mikoa mingine nchini.

Akitoa tamko hilo mbele ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo Mahiza amesema mkoa umeamua kuzuia kabisa uingizaji wa mifugo yoyote  ndani ya mkoa huo kwa ajili ya malisho kutokana na migogoro na mapigano ya mara kwa mara yanayotokea kati ya wakulima na wafugaji.

Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa amesema usitishaji na uzuiaji wa mifugo inayoingizwa katika mkoa huo haihusu mifugo inayosafirishwa kwenda mikoa au nchi jirani kwajili biashara bali inahusu mifugo inayoingizwa kwajili ya malisho.

Mahiza amesema tayari amemuandikia barua  waziri wa mifugo Dokta David Matayo kumueleza kusudio hilo.

Tamko la kuzuia uingizaji wa mifugo kwa mkoa  wa Pwani linakuja ikiwa ni wiki mbili tu zimepita tangu kuzuka kwa mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji katika mji wa ikwiriri wilayani Rufiji na kusababisha kifo cha mtu mmoja, uchomaji wa nyumba na uharibifu mkubwa wa mali.

Joseph chewale, TBC Pwani .

Last Updated ( Thursday, 07 June 2012 12:19 )  
Banner