Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. SHUKURU KAWAMBWA amewaagiza maafisa elimu kote nchini kuharakisha kusambaza muongozo mpya wa wizara hiyo unaoagiza wakuu wa shule za sekondari nchini kuwafanyia usaili wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Akizungumza na wanafunzi shule ya sekondari ya LUGOBA mkoani PWANI Waziri KAWAMBWA amesema wizara imeamua kuwafanyia usahili wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza ili kubaini uvumi unaoenea kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari hawajui kusoma na kuandika.
Waziri KAWAMBWA amesema iwapo atabainika mwanafunzi yoyote amechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza akiwa hajui kusoma wala kuandika wizara itachukua hatua za kinidhamu kwa mwalimu mkuu wa shule aliyotoka mwanafunzi huyo pamoja na afisa elimu wake.
