Mbunge wa Kilombero ahukumiwa miezi sita jela
Mahakama ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro imemhukumu kifungo cha miezi sita jela mbunge wa jimbo la Kilombero Peter Lijualikali kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki.
Mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali

Mahakama ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro imemhukumu kifungo cha miezi sita jela mbunge wa jimbo la Kilombero Peter Lijualikali kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki.

 

Mwendesha mashtaka Inspekta wa Polisi Dotto Ngimbwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na mwenzie Stephano Mgata walitenda kosa hilo Machi Mosi mwaka 2016 eneo la Kibaoni katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

 

Ngimbwa amesema washtakiwa hao kwa pamoja walifanya fujo kinyume na kifungu namba 89 kifungu kidogo cha kwanza B,cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

 

Amesema mnamo Machi mosi mwaka 2016 saa nne asubuhi maeneo ya Kibaoni katika  ukumbi wa halmashauri washtakiwa walifanya fujo na kusababisha uvunjifu Wa amani katika eneo hilo.

 

Washtakiwa walikana mashtaka  na hivyo kufanya kesi kusikiliza ushahidi Wa pande zote mbili na upande Wa mashtaka ukathibitisha shtaka bila kuacha shaka.

 

Hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya Timothy Lyon amesema mahakama imewatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshtakiwa Wa kwanza(Mbunge) ambaye alikuwa na kesi tatu huko nyuma na kutiwa hatiani na kuhukumiwa yeye amehukumuwa jela miezi sita.

 

Lyon alizitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa ni kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014.

 

Amesema mahakama kwa kuona mshtakiwa ni mzoefu na katika kesi zote katiwa hatiani hivyo mahakama imeona mtuhumiwa ana hatia na anastahili kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

 

Hata hivyo mahakama hiyo imeona kwa kuwa mshtakiwa Wa pili hii ni Mara ya kwanza amehukumiwa kifungo cha miezi sita nje ambapo ndani ya kipindi hicho cha miezi sita hatotakiwa kutenda kosa lolote la jinai.

 

 

MONICA LIAMPAWE

JANUARI 11, 2017

MOST POPULAR
+
+
HABARI ZINAZO HUSIANA
ZILIZOSOMWA ZAIDI