Responsive image
Responsive image
Posted : May 10, 2018 (2 weeks ago) By TBC
Responsive image
David Goodall (104) ambaye amefanikiwa kusaidiwa kufa
Responsive image

Raia wa Austrialia mwenye umri wa miaka 104, David Goodall, amefanikiwa kutimiza azma yake ya kusaidiwa afe, kwa vile amechoka kuishi katika adha na ‘mateso’ yanayotokana na uzee.

Goodall amekufa baada ya kuchomwa sindano maalum ya sumu na madaktari wa kliniki inayoitwa Life Circle iliyoko Basel, swisi, ambako sheria zinaruhusu mtu kusaidiwa kufa kitaalam kama kuna sababu za msingi zinazomsukuma kuamua kufanya hivyo.

Mwakilishi wa taasisi ya Exit international inayopigania sheria ya ‘kusaidiwa kufa’ ipitishwe katika nchi zote duniani,  amesema kuwa Goodall alikufa huku akisikiliza ala za muziki maarufu unaoitwa ‘Ode to joy’ ulioboreshwa na mpiga piano wa Ujerumani Ludwig Van Beethoven mwaka 1824.

Mtunzi wa mwanzo kabisa wa muziki huo (kwa kijerumani  "An die Freude") alikuwa ni  mshairi wa Ujerumani pia  Friedrich Schiller aliyeandika shairi lenye hisia kali la ode to joy mwaka 1785.

Mwaka 1972 Baraza la nchi za Ulaya lilipitisha tuni ya wimbo huo iliyoboreshwa na Beethoven kama wimbo rasmi wa nchi za Ulaya na baada wimbo huo ulikuja kuidhinishwa na kinachoitwa sasa Umoja wa nchi za Ulaya (EU)

Goodall aliyeacha wajukuu 12, alilazimika kwenda Uswisi baada ya kushindwa kupatiwa huduma ya kusaidiwa kufa nchini kwake Australia ambako sheria haziruhusu jambo hilo.

Katika kampeni yake huko Australia alifanikiwa kupata michango iliyofikia Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa watu na taasisi mbali mbali zilizomwezesha kusafiri hadi Uswisi.

Katika mahojiano siku mbili kabla ya kifo chake Goodall alisema maisha yake yalikoma kuwa yenye furaha kiasi cha miaka mitano au 10 iliyopita kutokana na madhaifu kadhaa ya mwili yakiwemo ya kushindwa kuona na kutembea.

Goodall ambaye kitaaluma alikuwa ni mtaalam wa ikolojia alisema alipokuwa na nguvu alikuwa akitumia muda mwingi kwenye mapori na misitu akifanya tafiti na angependa kwenda huko tena kusikia ndege wakiimba na kuona mazingira ya porini, lakini hawezi tena.

Alisema ana matumaini kuwa hatua yake ya kusaidiwa kufa itasaidia kufanya haki hiyo iweze kupatikana katika nchi nyingi zaidi duniani.

" Ninafurahi kwamba kwa kipindi kirefu cha nyuma nimekuwa nikihojiwa na waandishi wa habari na nimeweza kulifanya suala hili liingie kwenye mjadala “ alisema.

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment