Responsive image
Responsive image
Posted : May 09, 2018 (2 weeks ago) By TBC
Responsive image
Rais Donald Trump wa Marekani
Responsive image

Rais Donald Trump wa Marekani amethibitisha katika hotuba iliyokuwa ikisubiriwa na wengi jana kwamba Marekani inajitoa katika mkataba wa kuiondolea vikwazo vya kiuchumi Iran uliosainiwa na mataifa makubwa na nchi hiyo, mwaka 2015.

Mkataba huo uliofahamika kama Joint Comprehensive Plan of Action (JCPOA) uliondoa vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vimewekwa na Umoja wa Mataifa, Ulaya na  Marekani dhidi ya Iran kwa sharti kwamba nchi hiyo iachane na uwekezaji mkubwa uliokuwa unafanywa kwenye madini ya Uranium ambao dunia ilihofu kwamba ulikusudia kujenga uwezo wa kutengeneza bomu la nuklia.

Rais Trump ambaye kwa uamuzi huo amejenga ufa kati ya Marekani na washirika wake wa kihistoria wa Ulaya, ameuita mkataba huo uliokuwa umeasisiwa na mtangulizi wake, Barack Obama, kuwa ni mkataba uliooza unaomletea shida yeye kama raia wa Marekani. Baadhi ya mataifa ya Ulaya yaliyomo kwenye mkataba huo yanafanya biashara kubwa na Iran katika sekta za mafuta na benki kufuatia kuondolewa kwa vikwazo chini ya mkataba huo.

Trump amesema atarudisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran vilivyokuwa vimeondolewa na mkataba huo kwa madai kwamba nchi hiyo imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kupunguza uwekezaji katika nuklia na kuruhusu upekuzi, kama ilivyokuwa imeanishwa na mkataba huo.

Trump pia amedai kuondolewa kwa vikwazo kumeifanya Iran kujipatika pato kubwa kutokana na biashara na kutumia fedha nyingi katika kuvisaidia vikundi vya ugaidi duniani.

Kwa upande mwingine mataifa makubwa matano yaliyobaki katika mkataba huo, Russia, Ufaransa , China, Ujerumani na Uingereza yote yamekubaliana kwamba hakuna haja ya kurejesha vikwazo dhidi ya Iran kwa vile mkataba huo ulikuwa unatekelezwa vizuri na Iran kama ilivyokuwa imepangwa.

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema  nchi yake itaendelea kuzungumza na mataifa yaliyobaki kwenye mkataba huo katika siku chache zinazokuja, na kama itaona uamuzi wa Trump umebadili msimamo wa mataifa hayo, itaanza uwekezaji wa nguvu katika Uranium.

Amesema kuwa lakini kama mataifa hayo yatapuuza msimamo wa Marekani na kuendelea kushirikiana na Iran, nchi hiyo ipo tayari kupunguza uwekezaji katika Uranium kwa mujibu wa kalenda iliyowekwa chini ya mkataba wa mwaka 2015.

"Nimeiagiza taasisi ya atomiki ya Iran ijiandae ili kama itakuwa lazima basi tuanze tena uwekezaji wa nuklia kwa ajili ya matumizi ya viwanda na bila mipaka yoyote” amesema Rais Rouhani.

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment