Responsive image
Responsive image
Posted : May 03, 2018 (3 weeks ago) By TBC
Responsive image
Polisi wanaamini kuwa mlinzi katika eneo hili la Shirika la Msalaba Mwekundu alikula njama na watekaji
Responsive image

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema ofisa wake mmoja ambaye ni nesi ametekwa nyara na watu wasiojulikana nchini Somalia.

Watu wenye silaha walimteka Sonja Nientiet mwenye asili ya Ujerumani, nje ya jengo la Msalaba Mwekundu anapofanyia kazi, jana Jumatano majira ya saa 2 usiku kwa saa za Somalia.

Msemaji wa Serikali amesema wameweza kumtambua mlinzi mmoja wa jengo hilo anayeshukiwa kushirikiana na watu waliomteka nyara nesi huyo.

Mashuhuda wameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba walimuona mlinzi akiwasaidia watekaji kwa kumchelewesha Nietiet baada ya kumpakia kwenye gari iliyokuwa ikisubiri huku moja ya tairi zake ikiwa na pancha. Gari hiyo baadae ilikutwa na polisi ikiwa katika hali inayohitaji matengenezo, na wanaamini ilitumika katika njama za utekaji.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema linawahamishia Nairobi maofisa wake 10 wa kutoka nchi mbali mbali waliosalia hapo Mogadishu, hadi hapo taarifa nyingine itapotolewa.

Katika tukio lingine juzi Jumanne mwanamke raia wa Somalia anayefanya kazi katika ofisi za Shirika la Afya Duniani (WHO) mjini Mogadushu, aliuawa kwa kupigwa risasi.

Ndugu wa mwanamke huyo aliyefahamika kama Mariam Abdullahi Mohamed, amesema marehemu alishambuliwa akiwa sokoni akinunua bidhaa kwa maandalizi ya harusi yake iliyotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Hata hivyo, hapajakuwa na viashiria vinavyoonyesha kuwepo kwa uhusiano kati ya tukio hilo la mauaji na lile la utekaji nyara.

Polisi wanaendelea kumtafuta nesi aliyetekwa nyara. Haijajulikana bado waliotekeleza tukio hilo ni kina nani, lakini wapiganaji wa Al-Shabab wenye uhusiano wa karibu na kikundi cha Al-qaeda bado wamekuwa wakifanya mashambulizi ya hapa na pale, nchini humo.

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment