Responsive image
Responsive image
Posted : April 30, 2018 (3 weeks ago) By TBC
Responsive image
Eneo lililoshambuliwa kwa mabomu mjini Kabul, Afghanistan
Responsive image

Waandishi wa habari 10 ni miongoni mwa watu 31 waliokufa katika mashambulizi yaliyotokea leo Jumatatu huko Kabul, Afghanistan.

Shah Marai wa Shirika la Habari la Ufaransa linalojulikana kama ‘ Agence France Presse’ (AFP) ni miongoni mwa waandishi wa habari waliokufa baada ya mshambuliaji aliyejifanya mpigapicha wa Televisheni kulipua bomu la pili mahali ambapo bomu la kwanza lilikuwa limelipuka.

Kikundi cha ugaidi cha Islamic State kimedai kuhusika na mashambulizi yote mawili.

Mlipuko wa kwanza ulitokea majira ya saa mbili asubuhi kwa saa za huko, katika eneo la Shashdarak ambapo ni karibu na jengo la ubalozi wa Marekani na majengo ya serikali ya Afghanistan.

Mlipuko huo uliwafanya waandishi wa habari kukimbilia eneo la tukio, ndipo mshambuliaji aliyejifanya mpiga picha wa TV alipolipua bomu lingine, msemaji wa polisi wa mji wa Kabul, Hashmat Stanikzai, amesema.

Wengine waliouawa katika shambulio la bomu ni pamoja na Mahram Durani na Ebadullah Hananzai ambao ni waandishi wa  Radio Free Europe, Yar Mohammad Tokhi mpiga picha wa ToloNews, Ghazi Rasoul, mwandishi wa 1TV na wapiga picha Nawroz Ali Khamosh, Ali Saleemi and Saleem Talash kutoka Mashal TV. Pia Sabawon Kakar, mpiga picha wa RFE alikufa akiwa hospitalini akitibiwa majeraha.

Katika tukio lingine, mwandishi wa habari wa BBC wa idhaa ya Afghanistan, Ahmad Shah (29) amekufa baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akielekea nyumbani kwake katika jimbo la Khost.

Katika taarifa kupitia mitandao ya jamii kikundi cha ISIS kimemtaja mshambuliaji wa bomu la kwanza kuwa ni Qaqaa al-Kurdi na wa pili ni Khalil al-Qurshi. Hata hivyo Kikundi hicho hakikutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake ya kuhusika.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Mkurugenzi wa habari wa Shirika la AFP Michele Leridon, amemuelezea Marai aliyekuwa akiripoti mgogoro wa Afghanistan kwa ajili ya shirika hilo kwa zaidi ya miaka 15 kuwa ni mwanataaluma mahiri, mwenye ujasiri, upendo na dhamira ya ajabu.

“Kifo cha hazina yetu Shah Marai katika mabomu mjini Kabul ni pigo kubwa mno” amesema Leridon amnbaye ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waandishi wengine waliouawa katika mashambulizi hayo.

Marai aliajiriwa na AFP kama dereva mwaka 1996, mwaka ambao kikundi cha Taliban kilitwaa madaraka nchini humo, na mwaka 2002 alibadilishiwa kazi na kuajiriwa kama mpiga picha, ambapo aliweza kupanda ngazi hadi kuwa mpiga picha mkuu katika ofisi ya AFP Afghanistan.

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment