Responsive image
Responsive image
Posted : April 27, 2018 (4 weeks ago) By TBC
Responsive image
Responsive image

Polisi wa jimbo la California Marekani wamemkamata Joseph DeAngelo (72) anayetuhumiwa kwa matukio 12 ya mauaji, 51 ya ubakaji na zaidi ya 120 ya uvunjaji kati ya mwaka 1976 na 1986, yaliyoleta hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Sacramento, San Francisco, kati na Kusini mwa jimbo la California.

Polisi wanaamini kuwa DeAngelo ndiye mtu ambaye katika miaka hiyo alipachikwa majina kama vile the Golden State Killer, the East Area Rapist, Original night stalker na Diamond Knot killer ambayo kwa tafsiri nyepesi ni ‘muuaji wa jimbo la California’ (ambalo pia huitwa Golden State), mbakaji wa eneo la mashariki, mnyatiaji halisi wa usiku na mnyongaji wa ‘kitanzi cha almasi” kutokana na aina ya fundo alilokuwa anatumia kunyonga kwa kamba wahanga wake.

Kwa miaka mingi polisi wamekuwa na taarifa za vinasaba (DNA) zilizochukuliwa kutoka kwenye maeneo ya matukio hayo lakini walishindwa kumtambua mhusika hadi hivi karibuni ambapo kwa mujibu wa Steve Grippi, Mwendesha Mashitaka wa eneo la Sacramento,  waliunganisha taarifa zao za DNA na zile zilizokuwa zimewekwa kwenye tovuti zinazoendeshwa kusaidia watu waliopotelewa na wazazi, ndugu au jamaa kuwapata au kupata miili yao. Haijafahamika kama tovuti hizo zililazimishwa kutoa taarifa hizo au zilitoa kwa hiari.

Ofisa wa mradi mmoja wa DNA unaosaidia kufuatilia watu waliouawa ambao hawajatambuliwa na kuweza kuwarudisha kwenye familia zao, ameripotiwa akisema kuwa huenda taarifa za DNA zilizotumwa kwenye tovuti hizo na ndugu wa karibu wa muuaji, zilitoa fununu muhimu kwa polisi ambao sasa wakabakia na watu wachache wa kuwafuatilia.

Polisi pia walitumia mbinu nyingine kama vile za kukadiria umri wa mtu aliyekuwa akifanya matukio hayo na kisha wakaanza kumfuatilia DeAngelo ambapo walipochukua kipimo cha vinasaba vyake wakathibitisha kuwa vilikuwa ni sawa na vile walivyokuwa wamechukua kwenye maeneo ya matukio.

Polisi pia wamesema DeAngelo ambaye ni askari polisi wa zamani, alikuwa akiishi katika kitongoji kimoja huko  Sacramento, mahali ambapo ni karibu sana na maeneo ambapo mauaji kadhaa ya mwanzo yalifanyika.  

CHANZO BBC

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment