Responsive image
Responsive image
Posted : March 13, 2018 (2 months ago) By TBC
Responsive image
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani aliyeng'olewa Rex Tillerson
Responsive image

Rais wa Marekani Donald Trump amemuondoa madarakani waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Rex Tillerson (64), na kumteua Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Mike Pompeo kushika nafasi hiyo.

Rais Trump pia amemteua mwanamama Gina Haspel kuwa mkurugenzi wa CIA, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanamke kuongoza shirika hilo.

Tillerson, Mkuu wa zamani wa kampuni tajiri ya mafuta duniani, Exxon Mobil,ameshika wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje kwa takriban mwaka mmoja tu, tangu alipoteuliwa na Trump mwanzoni mwa mwaka jana.

Shirika la Habari la BBC limesema limedokezwa na ofisa mwandamizi wa Ikulu ya Marekani kwamba kwa kuangalia wakati ambao Trump ametangaza mabadiliko hayo, bila shaka Rais huyo anataka kuhakikisha kuwa timu yake mpya inaanza kazi kabla hajaingia katika mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika Mei, kati yake na Korea Kaskazini.

Wiki iliyopita Tillerson alitembelea Kenya, Chad na Nigeria ambapo akiwa katika ziara hiyo ya Afrika, nyuma yake Trump akatangaza kuwa atafanya mazungumzo na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Akiwa Afrika, Jumamosi iliyopita ghafla Tillerson alisema hajisikii vizuri na baadae Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ikatoa taarifa kwamba waziri huyo atafupisha ziara yake ya bara hilo kwa siku moja, jambo ambalo lilifanyika.

Wadadisi wamesema pamekuwa na hali ya kutofautiana mitazamo kwa muda mrefu kati ya Trump na mwanadiplomasia wake mkuu katika masuala mbali mbali hususan masuala ya Korea Kaskazini na Iran.

Mnamo Oktoba mwaka jana Tillerson alilazimika kuitisha mkutano na waandishi wa habari ili kukanusha taarifa zilizozagaa kwamba alikuwa anakusudia kujiuzulu, lakini hakusema chochote kuhusu taarifa nyingine ambayo nayo ilizagaa, kwamba aliwahi kumuita bosi wake mbumbumbu, baada ya kikao chao kilichofanyika wizara ya ulinzi ya Marekani (Pentagon) Julai mwaka jana.

Rais Trump naye aliwahi kusema hadharani wakati ule ambapo Rais Kim wa Korea Kaskazini alikuwa hajalegeza msimamo wake kuhusu silaha za nyuklia, kwamba Tillerson alikuwa anapoteza muda wake bure kujaribu kutafuta upatanishi na nchi hiyo.

Taarifa nyingine zimesema Tillerson alikuwa anashangazwa na kiwango kidogo cha uelewa alicho nacho Trump kuhusu sera ya mambo ya nje ya nchi hiyo, huku gazeti la New York Times likiwanukuu baadhi ya watu wakisema kuwa Trump alikuwa anachukizwa na ‘lugha ya vitendo’  aliyokuwa akiitumia Tillerson wakati wa vikao.

Imeelezwa kuwa Tillerson alikuwa na tabia ya kuzungusha macho yaliyoashiria dharau, pale alipokuwa hakubaliani na maamuzi ya bosi wake.

MACHI 13, 2018

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment