Responsive image
Responsive image
Posted : March 11, 2018 (a week ago) By TBC
Responsive image
Rais Xi Jingping wa China
Responsive image

Bunge la China limepitisha mabadiliko makubwa kwenye katiba ya nchi hiyo ambayo yanamsafishia njia Rais  Xi Jinping kuwa Rais wa maisha nchini humo.

Wajumbe wa bunge hilo maarufu kama National People's Congress (NPC) wamepiga kura kuhusiana na mapendekezo ya kubadilisha ibara mbali mbali kwenye Katiba, lilikiwemo la kuondoa ibara zilizokuwa zimeweka ukomo wa utawala wa Rais kuwa ni mihula miwili tu ya miaka mitano mitano.

Kati ya kura 2,964 zilizopigwa ni kura mbili tu zilizokataa pendekezo hilo,huku wajumbe watatu wakiwa hawakupiga kura yoyote,  jambo linaloashiria kuwa kama kutakuwa na upinzani katika safari ya Rais Xi kuelekea utawala wa maisha, upinzani huo utakiwa ni mdogo.

Rais Xi mwenye umri wa miaka 64 ni rais mwenye nguvu ambaye analinganishwa na muasisi wan chi hiyo Mao Zedong na mwenyewe anaonekana kuwa angependa kuwa Rais wa maisha kama alivyokuwa Mao.

Akizungumza wiki iliyopita, Rais huyo aliyabariki mapendekezo hayo ya Katiba huku akisema yanaakisi matakwa ya pamoja ya chama na wananchi wote wa China.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wachambuzi wamenukuliwa na Shirika la Habari la CNN, wakidai uamuzi huo huenda ukamletea shida kisiasa Rais huyo baada ya muda mrefu katika utawala wake wa maisha, kwani utakosa maslahi kwa taifa.  

LIkiwa na wajumbe takriban 3000 NPC ni Bunge lenye wabunge wengi kuliko Bunge lolote duniani. 

NPC ndio chombo kikuu kuliko vyote cha maamuzi nchini China kikiwa na mamlaka ya kubadilisha katiba, kutunga sheria na hata kuchagua Rais, Makamu wa Rais na viongozi wengine wakuu wa serikali na pia kuweza kuwaondoa madarakani.

Hata hivyo watafiti wanasema hali hiyo ipo kinadharia tu kwani mara zote NPC imekuwa ikitumika kama muhuri tu wa kubariki maamuzi yanayofanywa na serikali na Chama Cha Kikomunisti cha China.

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment