Responsive image
Responsive image
Posted : February 14, 2018 (2 months ago) By TBC
Responsive image
Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma:
Responsive image

Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma amelihutubia taifa hilo kupitia televisheni, ambapo ameeleza kusikitishwa kwake na jitihada za chama chake za 'kumkimbiza' kumtoa madarakani, jambo ambalo amesema halimtendei haki.

Alikuwa akizungumzia hatua ya Kamati Tendaji (NEC)  ya ANC ambayo juizi ilimpa saa 48 awe amejiuzulu au ang'olewe na Bunge kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye. 

Zuma alisema amekubali kuachia madaraka mwezi Juni mwaka huu kama ANC wangekubali hoja ya kufanya mabadiliko ya taratibu, lakini chama hicho kimekataa pendekezo hilo, jambo ambalo linamshangaza  ni kwa nini wanataka aondoke kwa haraka kiasi hicho.

Zuma amekanusha shutuma zinazoelekezwa kwake kwamba anakiletea kiburi chama cha ANC huku akisisitiza kwamba ni vyema aiongoze nchi hiyo kwa miezi kadhaa ili pamoja na mambo mengine, aweze kuyasimamia matukio ya kimataifa ambayo yeye ni Mwenyekiti kama vile mkutano wa viongozi wa nchi za BRICS.

"Haraka hii ni ya nini?. Hili jambo limetekelezwa katika namna ambayo ninahisi kuonewa" amesema Zuma.

Saa 48 alizopewa Zuma zinaisha leo Jumatano huku kukiwa hakuna dalili ya Rais huyo kung'atuka kwa hiari. 

Baadhi ya wajumbe wa NEC wamenukuliwa wakiendelea kusisitiza katika nyakati tofauti kwamba ni lazima Rais huyo aondoke, na habari zaidi zimesema tayari Spika wa Bunge amekubali kupokea hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Rais katika kikao cha Bunge kesho Alhamisi, ingawa hatua hiyo inapaswa kuridhiwa kwanza na Kamati ya Bunge.

Wakati hayo yakiendelea polisi wamevamia nyumbani kwa familia ya Gupta mjini Johanesburg na kuwakamata watu watatu ikiwa ni mwendelezo wa serikali kushinikiza uchunguzi dhidi ya familia hiyo inayodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa serikali ya Bw. Zuma.

Shirika la utangazaji la Afrika Kusini SABC limeripoti kuwa mmoja kati ya watu waliokamatwa ni kaka wa familia hiyo ya Gupta.

Familia hiyo tajiri yenye asili kutoka India wametuhumiwa kutumia urafiki wao na rais Zuma na kutumia urafiki huo kwa manufaa ya biashara zao. Rais Zuma na familia ya Gupta wamekana tuhuma hizo.

Msemaji wa polisi Haungwani Mulaudzi amesema wana matumaini kuwa ushahidi uliokusanywa utatosha kuifungulia mashitaka familia hiyo.

 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment