Responsive image
Responsive image
Posted : February 13, 2018 (3 months ago) By TBC
Responsive image
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Responsive image

Habari kutoka ndani ya chama tawala nchini Afrika Kusini zimesema kuwa kamati tendaji ya chama hicho imempa saa 48 Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kuachia madaraka vinginevyo atakabiliwa na hatua ya kung'olewa kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani itakayoanzishwa na chama chake cha ANC ndani ya Bunge.

Uamuzi huo umefikiwa na kamati hiyo (NEC) iliyoketi kwa takriban saa tisa kuamua hatma ya Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma ambaye amekuwa katika shinikizo la kuondolewa kwenye nafasi yake kwa tuhuma za rushwa.

Habari zimesema wakati NEC ikiendelea usiku jana, Makamu wa Rais Cyril Ramaphosa alionekana akiondoka na msafara wake kuelekea nyumani kwa Rais Zuma mjini Pretoria, ambapo alimfikishia ujumbe kuwa amepewa saa 48 kujiuzulu ili asikabiliane na kashfa ya kuondolewa madarakani na Bunge linalotarajiwa kuketi siku chache zijazo.

NEC haina mamlaka ya moja kwa moja ya kumng'oa madarakani rais huyo, lakini inatarajiwa kutumia ushawishi wake mkubwa ndani ya Bunge ambapo chama tawala cha ANC kina asilimia 62 ya viti, kumuondoa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Inatarajiwa pia kwamba wabunge wote wa vyama 13 vya upinzani nchini humo, wataungana na wenzao wa ANC katika kura hiyo ya kutokuwa na imani na Rais Zuma.

Zuma, mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akishinikizwa kuachia madaraka tangu mwezi Desemba mwaka jana baada ya Ramaphosa kushika nafasi kama kiongozi wa ANC.

 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment