Responsive image
Responsive image
Posted : January 12, 2018 (4 months ago) By TBC
Responsive image
Mchezaji bora wa Disemba Habibu Kiyombo
Responsive image

Mshambuliaji wa timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza, Habibu Kiyombo amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu Tanzania bara kwa  mwezi Disemba.

Kiyombo amechaguliwa kuwa mchezaji bora baada ya kuwashinda wachezaji wenzake wawili alioingia nao katika kiny’ang’anyiro hicho kutokana na tathmini pana iliyofanywa na kikao cha kamati ya tuzo.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao mawili katika mwezi Disemba, mwezi ambao kila timu ya ligi kuu Tanzania bara imecheza mchezo mmoja tu katika mzunguko huo wa 12.

Mabao hayo mawili aliyafunga katika mchezo dhidi ya Yanga,yaliyoipandisha Mbao kutoka nafasi ya nane hadi ya saba katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara huku nyota huyo akifikisha mabao saba msimu huu, akizidiwa bao moja tu na kinara Emanuel Okwi mwenye mabao nane.

Kiyombo amewashinda John Bocco wa Simba aliyefunga mabao mawili katika ushindi wa Simba wa magoli mawili kwa bila dhidi ya Ndanda Fc ya Mtwara, na Bruce Kangwa aliyeisaidia Azam Fc kupata ushindi wa magoli matatu kwa bila dhidi ya Stand United ya Shinyanga ambapo alifunga bao moja na kutoa pasi ya bao moja.

Nyota huyo atakabidhiwa tuzo, kisimbusi, cha Azam na Fedha taslim shilingi million 1 kutoka kwa wadhamini wa ligi kuu Tanzania bara.

Nyota wengine waliowahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi katika ligi kuu Tanzania bara tangu kuanza kwa ligi hiyo ni Emmanuel Okwi wa timu ya Simba aliyetwaa tuzo hiyo mwezi Agosti, Shafiq Batambuze wa Singida United aliyetwaa mwezi Septemba, Obrey Chirwa wa Yanga aliyetwaa tuzo ya mwezi Oktoba na Mudathir Yahya wa Singida United aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Novemba.

 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment