Responsive image
Responsive image
Posted : May 16, 2018 (a week ago) By TBC
Responsive image
Rais Kim Jong – Un wa Korea Kaskazini
Responsive image

Korea kaskazini imesema inaweza kujitoa katika mazungumzo kati ya Rais Kim Jong Un wa nchi hiyo na Rais Donald Trump wa Marekani yanayotarajiwa kufanyika Juni 12 mwaka huu, kama Marekani itaendelea kusisitiza kauli zake kuwa nchi hiyo iachane na silaha za nuklia.

Katika kauli zilizoonekana kujaa hasira, Makamu wa waziri wa mambo ya nje wa Korea kaskazini Kim Kye-gwan ameituhumu Marekani kwa kutoa kauli zisizo na umakini na zinazoonyesha nia mbaya, akimtaja moja kwa moja Mshauri wa Marekani wa mambo ya usalama , John Bolton. "Hatuwezi kuficha hisia zetu dhidi yake” amesema Kye-gwan.

Bolton anafahamika kuwa ni mtu mwenye kuamini katika ‘nguvu ya Marekani’ na anayepigania kuona nguvu hiyo ionekane ikitumika nje ya Marekani. Siku za nyuma aliwahi kunukuliwa akisema ingekuwa ni jambo la haki kabisa kufanya shambulio la kuichokoza Korea Kaskazini kabla haijafanya lolote.

Katika mahojiano na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Bolton amesema Korea Kaskani inaweza kufuata mtindo uliotumika Libya kuiondoa katika harakati zake za kuboresha silaha. Nchi hiyo iliacha kuboresha silaha ndipo ikapata msaada wa kiuchumi.

Kye-gwan amesema kauli hiyo haionyeshi kwamba kuna nia ya kutatua mgogoro huo kwa njia ya maongezi.

"Ni kauli zinazoidhihirisha  nia mbaya iliyokuwa imejificha ya kuifikisha nchi yetu tukufu katika hatma iliyoikuta Libya au Iraq ambazo zote zilianguka baada ya kujiweka kwa ukamilifu chini ya mataifa makubwa” amesema katika taarifa yake.

Makubaliano ya Rais Kim Jong-Un na Trump kukutana yalifikiwa wakati Korea Kaskazini ikisema kuwa ina nia thabiti ya kulifanya eneo la Peninsula ya Korea kuwa lisilo na nuklia.

Kwa mujibu wa Korea Kaskazini, kauli hiyo haikumaanisha kwamba nchi hiyo iko tayari kuwekewa masharti au kulazimishwa kutokuwa na silaha, kama kauli za Bolton zilivyoashiria.

Kauli ya Rais Kim iliyotangazwa na vyombo vya habari vya Serikali ilisema “kama Marekani inatutega (ili tuingie kwenye mazungumzo) na kisha peke yake ichukue hatua za kutaka kutulazimisha tuachane na nuklia, hatutataka kushiriki mazungumzo hayo na itabidi tutafakari upya kuhudhuria mkutano wa Juni 12”.

Korea Kaskazini imesema ilikuwa na matumaini makubwa lakini kwa bahati mbaya Marekani inawachokoza kabla ya mkutano huo kwa kutoa kauli za kuudhi.

Aidha saa chache kabla ya kutoa kauli hizo, Korea Kaskazini pia ilijitoa kutoka kwenye mazungumzo yaliyotarajiwa kufanyika leo Jumatano kati yake na Korea Kusini, baada ya Marekani na Korea Kusini kufanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja.

Korea kaskazini ambayo mara zote imekuwa ikisisitiza uwekezaji wake kwenye silaha ni kwa ajili ya kujilinda, imesema kuwa vitendo hivyo ni ishara ya uchokozi na vinabomoa juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na nchi hiyo. 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment