Responsive image
Responsive image
Posted : May 14, 2018 (a week ago) By TBC
Responsive image
Mamia ya wapalestina wamejeruhiwa katika ukanda wa Gaza baada ya kushambuliwa na jeshi la Israel. Picha na AFP
Responsive image

Wapalestina wasiopungua 43 wameuawa na wengine 2,200 kujeruhiwa leo Jumatatu katika ukanda wa Gaza, baada ya kushambuliwa na vikosi vya Israel, katika ghasia kubwa kuliko zote tangu vita vya Gaza vya mwaka 2014.

Ghasia hizo zimetokea wakati Marekani ikifungua ubalozi wake mjini Jerusalem, hatua iliyowaudhi wa Palestina ambao wameiona kuwa ni kuunga mkono utawala wa Israel katika mji huo wote, ambao upande wake wa Mashariki wapalestina wanadai kuwa ni wa kwao.

Kwa upande mwingine Rais Donald Trump wa Marekani katika ujumbe wa video ameipongeza hatua ya kufungua ubalozi akisema Israel ni nchi huru yenye haki ya kuamua mji wake mkuu lakini kwa miaka mingi dunia imeshindwa kutambua jambo hilo lililo wazi. Trump ameongeza kudai kuwa Marekani iko thabiti katika nia yake ya kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.

Waandamanaji wapalestina walirusha mawe na kuwasha  moto, huku jeshi la Israel likitumia wadunguaji kuwapiga risasi, wakati ambapo moshi mzito kutoka kwenye matairi yaliyochomwa ulikuwa ukifuka.

Wizara ya afya inayoendeshwa na kikundi cha Hamas katika ukanda wa Gaza imesema watoto ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.

Maandamano yanayoongozwa na Hamas ni sehemu ya kampeni ya wiki sita ya kupinga utawala wa Israel iliyopewa jina "Maandamano ya kurudi nyumbani" huku Israel ikisema maandamano hayo yanakusudia kuvuka mpaka na kuzishambulia jumuiya za waisrael wanaoshi karibu na mpaka huo.

 

 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment