Responsive image
Responsive image
Posted : March 23, 2018 (a month ago) By TBC
Responsive image
Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba
Responsive image

Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba amepokea ripoti ya uchunguzi wa sakata la korosho za Tanzania kukutwa na mawe na uchafu mwingine nchini Vietnam na kumuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo  kwa kushiriana na vyombo vya dola kuwakamata na kuwahoji Maafisa wa Taasisi zote zilizohusika katika mchakato wa usafirishaji magunia ya korosho kwenda nchini Vietnam.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo mjini Dodoma baada ya kupokea Ripoti  hiyo kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa timu iliyoundwa ili kuchunguza sakata hilo ambayo imewataja baadhi ya maafisa wa serikali waliosimamia mchakato mzima wa kusafirisha korosho hizo kwenda nchini Vietnam.

Baada ya kupokea malalamiko kutoka nchini Vietnam kuhusu korosho za Tanzania kukutwa na uchafu wa aina  mbalimbali ikiwemo mawe, serikali iliunda Timu ya uchunguzi ili kuchunguza mchakato mzima uliotumika kusafirisha korosho  kuanzia bandari ya Mtwara, Dar es salaam hadi nchini Vietnam.

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, makamu mwenyekiti Timu hiyo Kassim Mbufu  amekabidhi ripoti kwa Waziri wa  Kilimo ikiwa na mapendekezo kadhaa  ikiwemo suala zima la  matumizi ya 'scanner' katika bandari zote.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo pia ameshauri serikali kufanya mazungumzo na Serikali ya Vietnam na kuwaeleza hatua walizochukua ili kuzuia udanganyifu huo.

Aidha Waziri Tizeba pia ameahidi kufanya  mazungumzo na wabunge wa Vietnam wanaotarajiwa kuwasilli nchini hivi karibuni  kwa niaba ya serikali yao ili kuwaeleza hatua walizochukua ili kuzuia vitendo hivyo vyenye lengo la kuharibu soko la korosho kutoka Tanzania.

ANETH ANDREW

MACHI 22, 2018

 

Responsive image
HABARI ZINAZOHUSIANA
MAONI YA WASOMAJI

Leave Your Comment