Tanzania Broadcasting Corporation - (TBC)

Thursday
Sep 09th
Text size
  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size
Home Movies Ujasiri umenifikisha hapa

Ujasiri umenifikisha hapa

Sarafina Mshindo,Kutokana na jinsi alivyokuwa anajieleza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza, nilijikuta nikihamasika zaidi nifanye mahojiano naye ili niweze kujua ana kitu gani kipya atakachoweza kuwafanyia Watanzania.

Huyo si mwingine bali ni Sarafina Mshindo, ambaye ni mmoja wa washiriki wa Bongo Star Search aliyetokea mkoani Dodoma na Balozi wa Pepsi Tanzania ambaye alipata fursa ya kwenda Los Angeles Marekani kwa udhamini wa SBC Tanzania ambao ni watengenezaji wa vinywaji baridi vya Pepsi, Mirinda na Pineapple.

Sarafina kama lilivyo jina
lake alionekana kuwa mcheshi na mwenye furaha wakati wote, jambo lililonitia hamu ya kumuuliza kulikoni hata wakati alipokuwa amewekwa kiti moto na waandishi wakati anaulizwa maswali alionekana ni mtu wa kujiamini zaidi.

“Siri ya yote haya ni kujiamini kwa kila jambo, siku zote nimekuwa nikiamini hivyo na ndio maana niliweza kushiriki kwenye michuano ya BSS ya mkoani
Dodoma tulikuwa washiriki wengi, kati ya 2,900 wasichana tulikuwa 900 tu na niliweza kushiriki kwa ujasiri,” alinieleza Sarafina wakati nilipofanya mahojiano naye kwa takribani saa moja jijini Mwanza.

Sarafina, ambaye ni mtoto wa mwisho wa familia ya marehemu Mzee Mshindo akiwa ni mchanganyiko wa Mbena upande wa baba na Mgogo upande wa mama, alizaliwa miaka 25 iliyopita mkoani Dodoma ambapo aliingia jijini Dar es Salaam na kuanza kufahamika kutokana na mashindano ya Bongo Star Search na kufikia hatua ya kumi bora.

Ndugu zake wengine ni Gladys ambaye ni pacha wa Elisha, wengine ni Charles na Patrick ambao wote wanaishi mkoani
Dodoma wakifanya biashara (Tripu) za uendeshaji wa magari makubwa kwenda nchi za Burundi, Rwanda na Zambia .

Ila anasema Gladys ambaye ni dada yake mkubwa yeye ni mfanyabiashara na mama yake Martha Yohana Mshindo yeye ni mama wa nyumbani.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chamwino,
Dodoma mwaka 1992-99 na kujiunga na Sekondari ya City ( City High School ) ambapo alisoma hadi kidato cha sita na baadaye akaanza kujishughulisha na muziki.

Anasema kipaji cha muziki kilianza wakati akiwa mdogo shuleni, alikuwa anaimba kwa kuwaiga wanamuziki wa ndani na nje ya nchi na mazoezi ya kuimba muziki yalikuwa yanachukua sehemu kubwa ya maisha yake.

Anasema alikuwa anapendelea kuimba zaidi nyimbo za wanamuziki wa nje ya nchi. “Kuna wakati nilikuwa natofautiana na mama hasa pale alipokuwa ananielekeza nifanye kazi fulani, lakini niliendelea hivyo hivyo baadaye akaamua kuniunga mkono na hata kaka zangu na dada yangu pia wote waliamua kuni-suppport,” anasema.

Sarafika anasema baada ya kuanza mchakato wa kushiriki kwenye mashindano ya Bongo Star Search, kuna watu wa karibu hususani marafiki zake waliokuwa wanamkatisha tamaa lakini anasema alikuwa na moyo wa ujasiri, hali ambayo ilimfanya aweze kushiriki hadi mwisho.

“Sasa kama nisingekata tamaa na kuonesha ujasiri wangu nisingeweza kufika hapa nilipo na nisingeweza kwenda nje ya nchi, na huko nimeona na kujifunza mengi, na nimeamini mwanamke wa Afrika akiwa jasiri anaweza kufanya mambo makubwa kuliko hata wanawake wengine wa nje ya Afrika,” anaeleza.

Sarafina, ambaye pia anapenda mchezo wa riadha, anasema kuwa kitu asichopenda katika maisha yake ni kukatishwa tamaa ya kutofanya jambo fulani ambalo yeye anaona anaweza kulifanya.

Anasema mtu anayemkatisha tamaa mtu asiweze kufanya jambo hakika anapoteza kipaji cha mtu huyo na kubainisha kuwa anamrudisha nyuma kimaendeleo na anawataka watu wa jinsi hiyo wasiwe wanawakatisha wenzao tamaa ya kushiriki kwenye jambo fulani.

“Unapomkatisha mtu tamaa ‘automatically’ utakuwa umekwamisha mambo yake, ni vema ukampa moyo kuliko kumfanyia hivyo, na hata mie binafsi nilipoanza kushiriki kwenye BSS Dodoma kuna marafiki zangu wa karibu walianza kunikatisha tamaa kwa kuniambia kuwa sitaweza, na ningefuata maneno yao ningekwama,” anasema.

Anasema asingekuwa jasiri asingeweza kupata fursa ya kukutana na wasanii mbalimbali wakiwemo Ike kutoka
Nigeria, Rachel (Uganda), na wengine kutoka Marekani, Holland, Afghanistan ambao watashiriki katika kuimba wimbo maalumu wa “Oooo Afrika,” kwenye ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini.

“Na hiyo ni baada ya kushiriki kwenye BSS na kuchaguliwa kuwa Balozi wa Pepsi, ujasiri na kujiamini vimenifanya kupiga hatua zaidi,” anasema.

Anasema katika maisha yake ni kuwa na furaha, huku akipewa fursa ya kusikilizwa matatizo yake ambapo anasema hupata nafasi ya kuelezea hisia zake bayana bila ya hofu yoyote ile.

“Nikipata nafasi hiyo ya kusikilizwa, nina imani kuwa watu watanisikiliza lakini pia watajenga kuniamini,” anaeleza.

Kwa humu nchini anatamani kuwa kama Mwanamuziki Lady Jay Dee, na kwa Bara la Afrika anatamani awe
kama Miriam Makeba na kwa duniani anatamani afanye kazi ya muziki afikie kiwango alichofikia mwanadada Whitney.

Anapendelea kula chips na samaki fresh na matunda kama vile ndizi na tufaa (apple) na anawashauri wasichana wasanii wa aina zote wa Kitanzania wahakikishe kuwa wanajiamini pindi wanapofanya shughuli zao ili waweze kuinyanyua sanaa ya
Tanzania.

Anasema kwa upande wa fani ya urembo nchini, kuna hatua nzuri iliyofikiwa ya kujivunia kama nchi kutokana na jinsi ambavyo mashindano hayo yamekuwa yanaandaliwa kwa hivi sasa lakini akasema mashindano ya mitindo (modelling) bado hayajapewa nafasi
kama yalivyo katika nchi nyingine duniani.

Sarafika anasema serikali imeweza kwa kiasi fulani kuweka juhudi kwenye upande wa muziki lakini anasisitiza kuwa iweke juhudi pia kwenye michezo mingine na uboreshaji zaidi wa kazi za wasanii.

Anasema matarajio yake ya baadaye ni kufanya kazi ya mitindo nje ya nchi, lakini pia anasema kuwa sio nia yake kufanya hivyo ni kutokana na mazingira halisi ya
Tanzania lakini dhamira yake kuu ilikuwa ni kuifanya kazi hiyo humu nchini.

Sarafina anasema kuwa matarajio yake ya baadaye ni kuwa na familia ya watoto wawili, ambapo hakusita kumuweka bayana mume wake mtarajiwa (mchumba) Alex Mashad ambaye kwa hivi sasa anaishi
Boston.

“Amekuwa ni mtu wa msaada
sana kwangu, na kila nilichokifanya tulikuwa tunawasiliana naye kwa karibu sana, na amekuwa akinitia moyo. Mungu akipenda tutafunga ndoa naye na matarajio yangu ni kuwa na familia ya watoto wawili,” anasema.

Anatoa shukurani za dhati kwa wazazi wake, hususani mama yake mzazi Martha, SBC Tanzania kwa kumuibua na kumfikisha hapo alipo na Benchmark Production Tanzania chini ya Madam Ritta Paulsen kwa jitihada kubwa waliyoifanya kwa kumuwezesha kwenye Bongo Star Search.

“Kwa namna ya kipekee navishukuru pia vyombo vyote vya habari kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kunitangaza, naamini bila ya vyombo hivyo nisingeweza kufika hapa nilipo navishukuru
sana,” anasema.

Huyo ndiye Sarafina Mshindo, ambaye ni kinda anayetarajiwa kutumbuiza wimbo maalumu wa “Oooo Afrika, kwenye michuano ya Kombe la Dunia, Afrika Kusini kwa kushirikiana na wasanii wenzake kutoka baadhi ya nchi za Afrika.

 
Banner