Ukitaka kujua mbuga ipi ina wanyama wengi tembelea
Nipo nyumbani kwangu nafanya shughuli zangu za hapa na pale, angalau kumaliza majukumu yote ya nyumbani, mimi kama mama wa familia angalua niweze kuweka mambo sawa kwa siku hii ya jumapili kwani Jumatatu hadi ijumaa natakiwa kuwepo kazini kutekeleza majukumu yangu ya kujenga taifa letu la Tanzania.
Namaliza vijikazi hivyo vya siku hii ya leo na gafla nasikia mlio wa simu ukiita alafu unakata, nahisi kuwa hao ni watu tu wakinitafuta kujua je nambari yangu ipo hewani au la. Mara nasikia simu inalia tena na kukatika. Mara ya tatu simu yalia tena natambua kuwa hapo inawezekana yule anayenitafuta ni mtu muhimu na ana jamboa la umuhimu sana. Naacha kuosha vyombo vyangu, najifuta mikono yangu angalau niweze kuipokea simu hiyo vizuri maana nikipokea simu na maji yanaweza kuiharaibu simu yangu ya ngama, nikajiingiza katika gharama za kununua simu zisizo na ulazima.

Simu yangu ni shilingi 15000 na simu ya tochi, ah naipenda sana mwaya. Naishika simu yangua ya kiganjani nasikia sauti ya rafiki yangu wa muda mrefu niliyewahi kusoma nae sekondari enzi zile za kujifunza kimombo kidato cha Kwanza Zanaki sekondari tukijifunza vitabu vya Mabala the Farmer na Hawa the Driver.

Si unatambua kuwa mambo ya kiingereza cha ugoko kama wanavyosema Wagosi wa Kaya, lakini Kiingereza tulijifunza na tukakijua. Msomaji wa tovuti ya TBC namsikiliza kwa makini sana, ninajulishwa kuwa baada ya juma moja atafunga ndoa na ndoa yake itafanyika huko Tanga ambapo yeye ni mkazi wa huko Mtae Lushoto ndipo asili yake akaniomba kuwa mie na mwezangu angalau tuwe wasimamizi wa shughuli yake. Hiyo ni Heshima kubwa, nimepewa na shoga yangu, lakini nikitambua kuwa usimamizi wa ndoa hii maana yake kuwa kuanzia leo najitishwa jukumu la uhakimu kusuluhisha pale migogoro ya ndoa itakapo tokea.

Maana mambo ya ndoa yana chungu na tamu zake. Namjibu kuwa nitafanya hivyo. Nafanya maandalaizi ya hapa na pale najiandaa angalau kupata viwalo vya harusi, si unatambua kuwa sie wanawake na urembo ni chanda na pete.

Nazunguka madukani kupata gauni kulingana na rangi niliyojulishwa. Siku moja kabla ya siku yenyewe nilipanda basi Ubungo Dar es Salaam hadi Mtae-Lushoto, ni mwendo mrefu wa zaidi ya saa 10. Huku Trafiki wakijaribu kutusimamisha hapa na pale lakini Dereva wa basi tuliopanda inaonekana na mwenyeji wa njia hii maana alikuwa akizungumza vizuri na polisi na kumalizana bila ugomvi ata kama tulikuwa tumevunja sheria za usalama barabarani.

Watu wanauliza njia wakati wa kwenda tu, wakati w akurudi kila mmoja mwenyeji. Nilifika huku na kuweza kufanya jukumu nilikabidhiwa, jioni ya siku husika tulifika katika mojawapo ya nyumba za ibada ambapo ndoa ilifungwa huku mie na mwezangu tukishiriki kwa nafasi yetu angalau kuwaingiza kataika ulimwengu wa ndoa na kifamilia ndugu hawa wawili. Usiku ulipotimia kila mmoja alipatiwa pahala pa kulala, kwa kuwa na mimi huku ni mgeninilipatiwea chumba jirani na kwa bibi na Bwana wa harusi. Nililala usingizi mzito mno mara baada ya uchovu wa siku hiyo. Ukitegemea kuwa nilikaribishwa na baridi nzito ya maeneo haya ya milimani.

Ilipokaribia alfajiri ya siku inayofuata niliamshwa na hodi, mwanzoni nilidhani ninaota kumbe ilikuwa hodi ya mabibi watatu. Kulikoni tena maajuza hawa asubuhi yote hii? Nilijulishwa kuwa na mama wa bibi harusi naye alikuwapo pamoja na shangazi yake alkaini hawakuwa jirani, Je wanataka nini? Kuna ugomvi alfajiri yote hii. Nilijulishwa kuwa wamekuja kupiga vigelegele vya harusi kama imejibu, nilipewa jukumu la kumuita bibi harusi kulijibu swali hilo. Duu kazi kweli kweli, basi niliwajibika kugonga mlango wa bibi na bwana wa harusi nailipokewa na ukimya kidogo.

Baada ya sekundi kama 120 nilisikia karibu ya sauti ya bibi harusi, ikisema karibu. Nilimuuliza swali hilo kama nilivyotumwa. Swali zito kutokana na kiza cha muda huo sikujua kama rafiki yangu niliyesoma nae kama alikunja uso au la, bali nilijibiwa nani anauliza? Nikajibu kuna mabibi wawili, rafiki yangu akasema achana nao. Nililipeleka jibu kwa mabibi hawa lakini nilirudishwa tena kuuliza swali hilohilo lakini sasa wakisema wanataka mzigo wao. Nilirejea tena chumba cha maharusi lakini sikupata ushirikiano. Ndipo alipokuja bibi mmoja mwenye ukakamavu kidogo akaniulizwa wewe si mzaliwa wa Tanga nikasema ndiyo mama, mie mswahili. Akasema sasa mwanakwetu huku kwetu ukiwa msimamizi wa mambo haya majukumu yako ndiyo haya, sio unashangashanga tu.

Bibi huyu shupavu aliwaita bila ya woga maharusi hao na kuwauliza swali lile lile alilonituma na kupata majibu yake.Wakatoka na kitu kikiwa kimefichwa na maharusi wakarejea chumbani kwao. Nilitoka nje na na mabibi hawa wakizungumza lugha ya asili ya watu hao ambao kwa hakika sikuifahamu kabisa baada ya muda wa dakika kadhaa mabibi hawa walikaa chemba. Wakalijadili jambo fulani na baada ya muda nilirudi chumbani kwangu nilipokuwa nimelala baada ya muda niliitwa nje tena na bibi mwingine ambaye alikuwa mswahili mzuri, akizungumza Kiswahili sahihi chenye kueleweka.

Bibi alinijulisha kuwa mwaya hapa kwetu bibi harusi akiolewa ni jambo la muhimu familia ya mama yake na ya bwana harusi kutambua kama binti huyo alikuwa bikira basi familia ya bibi harusi ukabidhiwa zawadi kedekede za heshima ili kuweza kuonyesha heshima kwa kumtunza binti huyo vizuri hapo vigelegele hupigwa na ndipo majirani hujaa. Akili kichwani mwako, familia huendelea na sherehe kubwa kutokana na tukio hilo la heshima kwa familia yao. Kinyume chake watu huondoka kimya kimya kwani binti huyo hana ubikira na ata famlia yake inatazamwa kwa jicho baya kwa kukosa uaminifu huo.

Hayo msomaji wa TBC Taifa ni mambo ya Tanga hayo, niliamka kulipokuchwa na kupanda basi kutoka Mtae Tanga na kurejea jiji la Mzizima. Lakini nilijifunza mengi kuwa ukitaka kujua mbuga ipi ina wanyama wengi basi lazima kuitembelea mbuga hiyo. Lakini uaminifu ni jambao la msingi kwa kila pahala.

Unaweza kuzisikiliza makala hizo hapo chini
Msomaji Studioni:   |   Frank Kashonde
Mwandishi:   |   Katherine Nchimbi
Mhariri   |   Adeladius Makwega
Unaweza kusikiliza makala haya hapo chini
MOST POPULAR NEWS