Mali ya umma na Wajinga ndiyo waliwao
Palitokea mtu mmoja katika kisiwa cha Unguja, enzi za Seyid Majid Bin Said, naye akikaa mjini. Na mtu huyu alikuwa hana kazi maalum, kazi yake ilikuwa ni kuwafuata Waarabu wakubwa wakubwa, na kupata manufaa yake kwao. Na kazi ya zamani hizo ilikuwa watu kufunga bidhaa na kwenda bara kufanya biashara, na kulima vyakula na kuuza.

Na yeye alikuwa mtu mmoja asiyetaka kazi ya namna hii. Hata hatima akaonelea mji hakukaliki. Akatafuta kanzu yake njema akavaa, na kilemba chake cheupe, na msahafu wake kwapani, akashika njia kwenda pande za mashamba kutarazaki. Na kazi aliyoichagua ni kazi ya ualimu kusalisha watu. Lakini yeye hajui kusoma hata herufi moja. Alichagua kwenda shamba kwa Wahadimu kwa kuwa huko ndiko walikokuwa wajinga wasiojua kusoma, na hata dini ya Kiislamu ilikuwa haijaingia kwao bado.

Basi Mwalimu akawasili Unguja Ukuu. Wahadimu walipomwona mgeni wakamkaribisha sana. Hata waliposikia kuwa yeye ni mwalimu wakazidi kumkaribisha na kumheshimu. Na yeye mwenyewe ikawa mchana kutwa kufunua msahafu,kurasa moja na nyengine kutazama tu, watu wanadhani anasoma!

Akapewa nyumba bure na chakula kwao. Hatima akawaambia, Jengeni msikiti nikusalisheni. Wahadimu wakajenga msikiti. Hata wakati wa kusali ulipojiri mwadhini hapana, maana wale wenyeji hawajui.

Basi ikawa kazi ya mwenyewe Mwalimu kuadhini. Lakini naye vilevile hajui kitu. Akasimama akaadhini hivi:- Allah Akbar! Allah Akbar! Wajinga ndio waliwao, Wajinga ndio Waliwao. Allah Akbar ! Watu wakajaa msikitini. Huyu mwalimu kama nilivyosema hajui kusoma, hajui kuandika na pia hajui kusalisha! Lakini watu wamekwisha kuwamo msikitini, ikawa hana hila ila kusalisha. Akaenda panapo Kibla, akasalisha hivi:- M, m, m,m ,m,m Wajinga ndio waliwao, Amin.

Ikawa kila akisema M,m,m ,m,m ,m ,m Wajinga ndio waliwao, Wajinga ndio Waliwao, Wahadimu huitikia Amin! Ikawa kila akiinama na kuinuka maneno ni hayo hayo. Na Wahadimu wakidhani asema Kiarabu, wakawa wamekazana tu, Amin! Zilipokwisha sala wakatoka nje. Wahadimu wakamsifu sana mwalimu wao jinsi anavyosalisha vizuri. Ikawa hivi hali ya mambo kwa siku nyingi kupita. Wakamfanyia mshahara mwema.

Siku moja akatoka Malimu wa kweli mjini anayejua kusoma na kusalisha ili kwenda kutembea shamba. Akafika Unguja Ukuu. Akapata habari kama mjini pana Mwalimu mmoja arifu sana, ndiye anayesalisha msikitini. Na huyu mwalimu mgeni asiende kumtazama, akangoja mpaka wakati wa sala.

Wakati wa sala ulipojiri akamsikia mwadhini anaadhini. Lakini maneno yake yakamstusha sana. Allah akbar! Allah akbar! Wajinga ndio waliwao. Allah akbar! Yule mgeni asiseme neno, akaenda msikitini, akakuta watu wamejaa. Na mbele yao panapo kibla yuko mtu anayemjua tangu mjini, naye kumjua kwake hajui kitu. Basi akamsogelea kule kule mbele ili amsikilize vema. Na mwalimu alipomwona huyu mgeni akastuka sana maana naye amjua tangu mjini.

Akawaza kuwa leo uongo wangu utabainika. Lakini mara akili zikamjia hivi:- M,m,m,m,m Mwalimu usinibaini, nikipata sita, tatu zangu, tatu zako, Wajinga ndio waliwao Amin! Na maneno haya wakisikiana wao wawili tu, maana walikaaa karibu karibu. Akashika kusalisha kwa maneno yale yale. M, m,m,m,m,m Mwalimu usinibaini, Wajinga ndio waliwao, nikipata nane, nne zangu na nne zako, Amin.

Akasalisha hivi mpaka mwisho, wakatoka. Walipotoka nje wale walimu wakaamkiana kwa vicheko sana. Watu walipowaona wanacheka,wakidhani wanacheka yao ya huku nje, maana wanajuana. Kumbe wanacheka yaleyale ya Msikitini: Mwalimu mwongo akisema Mwalimu usinibaini, wajinga ndio waliwao, nikipata nane, nne zangu, nne zako. Wakakaa katika hali hii wakiwala wajinga, mpaka walipochoka, wakaja zao mjini na wingi wa mapesa.

Hivi ndivyo ilivyo katika mambo mengi ya jumuiya na mambo ya umma. Mtaani kwetu tumechimba kisima cha maji matamu ya umma kwa msaada na huku sisi wananchi tukichangia nguvu zetu. Kisima kilipokamilika tukamchagua mmoja miongoni mwetu kusimamia kisima hiki na jukumu lake ni kukusanya pesa za mauzo ya ndoo moja moja ya maji tunayonunua ili kupata pesa za kulipia umeme.

Bwana kafanya kazi hiyo kwa miezi tisa kagawana na wajanja wenzake kisima kimeshindwa kufanya kazi na tumeshindwa kununua umeme kisima kimefungwa, je tuwafuate wafadhili watununulie ata umeme?

Lakini cha kustajabisha visima vya watu binafsi vinafanya kazi kila uchao na wenye visima wakikusanya mapesa na kuzidi kuboresha maisha yao. Hali hii ndivyo ilivyo katika mali nyingi za umma gharama kubwa zinatumika kununua mitambo na mashine ya viwanda vyetu na ata taasisi za umma lakini mara baada ya kazi kuanza wale wanaojita wajanja wanavunia mifukuni mwao, nikipata kumi tano zangu tano zako, wajinga ndiyo waliwao.

Je Mtanzania mwezangu tutaondokana lini na hali hii. Wanaofanya haya wako makini katika mali zao mno, hata kijana wa shamba akikamua maziwa na kuficha lita tano kati ya mia moja , aha mwanakwetu kibarua chake kitaota mbawa.

Je lini mali ya umma itaheshimika kama mali binafsi? Yule atakayetusaliti kwa kuchukua kumi, tano yeye na tano kwa jamaa yake tumfanye nini? Au tumuache kama wale wahadimu wa unguja ukuu?, na hakika msomaji wa tovuti yetu majibu ya maswali hayo matatu kwa leo, unayo mwenyewe mie sina.
Mwandishi:   |   Adeladius Makwega
Mhariri   |   Farida Hamisi
Unaweza kusikiliza makala haya hapo chini
MOST POPULAR NEWS