Mafundisho ya Shekhe wa Zanzibar
Napita hapa Mji Mkongwe Zanzibar nakutana na rafiki yangu wa muda mrefu ambaye nilisoma nae shule ya msingi Mkuranga enzi hizo. Namsabahi nayeye akiniuliza nimefuata nini Zanzibar? nikamjibu kuwa Zanzibar ni kwetu kwani ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nikaongeza kuwa hapo Zanzibar nina jamaa zangu wengi, akiwamo yeye ambaye nimesoma nae kipindi kile wakati tunajifunza kuumba herufi, darasa la kwanza. Unajua tena herufi zilikuwa zinapiga tikitaka. Kwa hakika walimu wetu wa darasa la kwanza wanafanya kazi mno.

Kwa kuwa nilikuwa sijaonana nae kwa muda mrefu akanichukua na kunipeleka hadi nyumbani kwake na kupata nafasi ya kuifahamu familia yake maana mara ya mwisho nilionana nae mwaka 1990 miaka 25 iliyopita, nimjuaye zaidi ni yeye, sasa mwezangu Mungu kambariki ameaminiwa kawa shekhe wa msikiti mmoja hapa Zanzibar.

Nilipata chakula cha mchana kwa haraka haraka kwani ndugu yangu huyu ana majukumu mengi ya kiroho sasa anafundisha katika Madrasat Al–Nuru, kama kawaida huwezi kuwa imam wa msikiti na mwalimu wa madrasa kama ni maamuma lazima uwe umemaliza juzuu kadhaa na elimu zaidi ya dini ya kiislamu.

Ndugu yangu huyu ni muumini na mshika dini sana na anatekeleza nguzo tano za dini hii. Mojawapo ya nguzo hizo ni ya kusali sala zote tano. Basi wakati wa salat ijumaa ulifika na niliambatana nae kuelekea msikitini japokuwa mimi si muislamu basi nilimsindikiza hadi jirani na msikiti huu ambapo niliona waumini wengi wakiingia na kufuata taratibu zote.

Kipindi hiki Zanzibar ilimpoteza msanii mmoja maarufu wa Tanzania na ata Afrika ya Mashariki. Kuna kipindi niliwahi kuwepo katika idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, niliona katika Wasanii wachache wa Afrika ambao kazi zao zilikuwa katika maktaba ya shirika hili ni kazi za msaniii huyu. Likiwa jambo la nadra sana kuweza kuona jina lingine la mwanamuziki wa Taifa letu.

Hii ni sifa kubwa huku nikidokezwa kuwa msanii alikuwa huyu anapewa mrabaha kila wimbo wake unapochezwa na shirika hilo la kimataifa duniani. Kumbuka kuwa ndugu yangu huyu aliingia msikiti, alisimama na kutoa tahadhari kwa wanadamu kuepuka kufa muflisi katika maisha ya dunia yetu kwa kutumia muda wetu katika shughuli zisizo na maana kwa maisha ya kesho.

“Ndugu zangu tuwe wazi na tuwe makini kwa kuwa hapa ulimwenguni tunayaandaa maisha ya kesho kwa kila tunalofanya. Sasa leo hii kila chombo cha habari kinamtaja masanii huyu aliyefariki dunia, kweli katangulia mbele ya haki, sawa! kama angekuwa anamuimbia mola basi kila ambapo ingekuwa wimbo wake unaimbwa basi kwa mola angekuwa anavuna mema. Sasa kila utakapoimbwa wimbo wowote wake anavuna mema? nawauliza sasa nyimbo zake zikiimbwa atavuna mema?”

Ndugu yangu aliuliza swali hilo mara mbili katika hotuba yake.

Alijibiwa kuwa hakuna mema yanayovunwa katika hilo.

“Tunatakiwa kusema bila ya kupamba kwani Kama hatufanyi mema na tuyafuata ya dunia basi tunakufa mufilisi huo ndiyo ukweli, ni jukumu langu mimi na wewe kuepuka kufa mufilisi yaani kufa ukiwa umefilisika kabisa, hauna kitu mbele ya Mungu. Watu leo hii tumekakalia ufisadi, dhuluma na mabaya mengi tunakufa muflisi” Alisisitika ndugu yangu huyu.

Alipomaliza hotuba hii akatoka nje ya msikiti huu na kuja pahala nilipo ilibidi nimuulize, kaka! inawezekana siku ya siku ata sisi tunaocheza nyimbo za kidunia redioni hatuwezi kuiona pepo ?

Rafiki yangu huyu kwanza akacheka sana akanijibu kwa kusema ha katekista Makwega, huko hakuna kwenda kwa hisani, huko unapimwa kwa mizani ya haki kwa kile ulichovuna.

Mahakama za huko hazina kumuonga jaji huko ni haki bin haki katekista Makwega. Shauri yako.

Nilimtania ndugu yangu achukue mlio wangu wa simu ambo ni kazi ya msanii huyu. Kwanza alicheka sana, alafu akasema ebu ucheze. Niliucheza mlio alafu akasema unasikia, unasikia kaka mie naweka kaswida tu, hiyo baki nayo mwenyewe.

Ustadhi rafiki yangu alinisindikiza hadi bandarini Zanzibar nikapanda boti nakurudi zangu bara angalau kuwahi majukumu yangu, maana mwajiri wangu sikumuwaaga juu ya safari yangu ya Zanzibar, vibarua vyenyewe vya sasa ni tabu mno.
Mwandishi:   |   Adeladius Makwega
Mhariri   |   Farida Hamisi
Unaweza kusikiliza makala haya hapo chini
MOST POPULAR NEWS