Warumi walitia chumvi historia ya Kleopatra wa Saba
Kleopatra lakini wako wengine hawalifahamu jina hili. Kleopatra ni mmojawapo wa watawala wa Misri wa kale, akifahamika kuwa ni mwanamke aliyeweza kuzikamata nyoyo za wanaume waliokuwa na mamlaka makubwa wakati ule wa utawala wa Rumi uliokuwa ukiitawala dunia, wakati huo, kama taifa kubwa la Marekani leo hii.
Kleopatra
Mwanamke kutoka Misri, aliyeweza kuutumia vizuri uwanamke wake kukamilisha kile alichokuwa anakiamini kuwa sahihi na kuweza kumteka kimawazo na kimapenzi Julius Kaisari, Mark Antony na wanaume wengine ambao walikuwa watawala wa dola kubwa ulimwenguni. “Maisha ya Kleopatra yalikuwa ya kushangaza mno, alikuwa ni malkia wa ajabu, mrembo aliyeweza kukamata mioyo ya watu wengi maarufu ulimwenguni.” Haya yanasemwa na Daktari wa Falsafa, Zahir Hawass, mtaalamu wa masuala ya kale kutoka Baraza la Mambo ya Kale nchini Misri. Unapotaka kuutambua ukweli juu ya jambo lolote ni vizuri kupata ushahidi wa watu zaidi ya wawili, kama wasemavyo wayahudi kuwa ushahidi wa watu wawili ni wa kweli lakini kumbuka unaweza ata kudanganywa na watu hao wawili wakati mwingine.

Unapotaka kutambua maisha ya Kleopatra wa saba ni vizuri kusikiliza kutoka upanda wa Misri na pia kusikiliza upande wa iliyokuwa dola ya Rumi ambapo kwa hakika mwanamke huyu imara aliwahi kuishi na watawala wa Rumi na kuzaa nao watoto; Julius Kaisari na Mark Antony.

Cleopatra wa Saba alizaliwa mwaka 69 kabla ya Yesu na alifariki Agosti 12 mwaka 30 kabla ya Yesu, alikuwa ni Farao wa Misri ambaye alifariki akiwa na umri mdogo mno. Huku jina Kleopatra likitokana na neno la kigiriki Kleopatra likimanisha mtu kutoka familia bora likisimama upande wa majina ya kike na kinyume ni Kleopatrols likimaanisha mwanaume.

Doktari Robert Steven Bianchi kutoka makumbusho ya Sanaa za Misri huko Tokyo Japan anatambua kuwa Warumi kwa sehemu kubwa walimtazama Kleopatra kwa jicho baya na jicho lisilo jema, jicho la kihasidi, tangu wakati ule, ata maandishi yao yanaonesha mtazamo huo lakini Kleopatra kwa sehemu kubwa amechangia mengi katika ustaarabu wa Misri na dola nzima ya Rumi.

“Warumi waliongeza chumvi katika simulizi ya maisha ya Kleopatra, walimsimulia kama mwanamke aliyejitongozesha kwa wanaume na kahaba mkubwa, aliyeweza kufanya mapenzi na mwanume yoyote wa Roma.” Kleopatra alikuwa na asili ya Ugiriki ya zamani baada ya utawala wa Axelander Mkuu kufariki wakati wa utawala wa Hellenistic ambapo katika uhai wake alikuwa akizungumza Kigiriki na alikataa katakata kuzungumza lugha ya Kimisri na wakati wa utawala wake Kigiriki na Kimisri zilitumika kwa pamoja kama lugha rasmi za mahakama.

Katika kuitawala Misri Kleopatra alitawala sambamba na baba yake na baadaye sambamba na kaka yake akishirikiana kwa karibu mno na Julius Kaisari ambaye alimjenga mno kuwa mtawala wa Misri na baadae kuzaa naye mtoto. Daktari Christina Riggs kutoka chuo Kikuu cha Mashariki mwa Anglia bado anamtazamo wa Warumi kuichezea historia ya Klepatra wa Saba.

“Ata umaarufu wa Kleopatra, yale tunayotambua ni simulizi tu, la muhimu kujua kuwa alikuwa mtawala wa Misri, ukipata ushahidi wa wamisri tutapata mtazamo wa utawala wa Kleopatra ulivyokuwa na si Warumi.” Waandishi na vyombo vya habari vinaweza kuliona tukio moja likasimuliwa kwa namna tafauti, kila mmoja akiwa na malengo yake kulieleza tukio hilo namna alivyopenda liwe, ndivyo ilivyokuwa kwa Warumi wa kale. Ikumbukwe kuwa Julius Kaisari aliuwawa mwaka 44 kabla ya Yesu huku Kleopatra akiungana na Mark Antony aliyejulikana kama Augustus walizaa nae watoto mapacha wawili Klepatra Selene II na Alexander Helios na baadaye wakazaa mtoto wa kiume mmoja. Baada ya kushindwa vita na Ocktavian, Mark Antony alijiua. Baada ya kifo hicho Caesarion mtoto wa Kleopatra na Julius Kaisari alijitangaza mtawala lakini punde tu aliuwawa kwa amri ya Octaviana na hapo hapo Misri ikawa sehemu ya Roma. Mama wa Kleopatra inaaminika kutofahamika lakini inahisiwa kuwa ni Cleopatra wa tano Kutokana na hali ya ufisadi na kutoa uhuru wa madaraka katika dola yake kulisababisha mapinduzi na kutolewa madarakani. Klepatra wa sita VI alifariki katika mazingira yasiyofahamika ambapo iliaminika kuwa alipewa sumu katokana na ushindani wa madaraka.

Mwaka 55 kabla ya Yesu Ptolemy Baba wa Kleopatra wa Saba alirejea akiwa na uungwaji mkono mkubwa wa Warumi na yule aliyesababisha kifo cha mama wa Klepatra alifungwa baadaye kunyongwa. Haya yote yakitokea Kleopatra wa Saba , tunayemzungumzia leo hii alikuwa na umri wa miaka 14 yaani mwali kabisa, akiwa msaidizi wa karibu wa baba yake, huku majukumu yake yakiwa madogo. Miaka minne baadaye Baba wa Kleopatra wa Saba alifariki dunia huku akiaacha wosia kuwa bintiye ambaye sasa alikuwa na miaka 18 tu na kijana wake wa kiume yaani kaka wa Kleopatra wapewe madaraka kwa pamoja. Miaka mitatu ya utawala wao ilikuwa migumu mno. Kwani nyota mbaya iliwaandama wakikumbwa na mafuriko kutoka mto nile, njaa kubwa na uchumi kwenda kombo.

Baadaye Kleopatra alikaa na kaka yake na kuwa mke na mume lakini alimzidi kete kaka yake na kutochangia mamlaka huku Kleopatra akiwa kinara wa madaraka. Basi msomaji wa makala haya hapa kwenye tovuti ya TBC unaweza kumalizia uhondo huo hapo chini. Unaweza kusikiliza muendelelezo wa makala haya katika kipindi cha Habari &Muziki kilichopo hewani TBC Taifa saa 12 jioni hadi saa1 Usiku

Unaweza kuzisikiliza makala hizo hapo chini
 
Mwandishi/Mfasiri   |   Adeladius Makwega
Mhariri   |   Katherine Nchimbi
Unaweza kusikiliza makala haya hapo chini
MOST POPULAR NEWS