Benki zetu na huduma za mashaka
Ni siku ya Ijumaa Januari 30, 2015 ninaamka mapema mno naelekea mjini kupata huduma za kibenki na si unatambu kuwa hivi sasa, karibu kila wilaya kuna benki kama ilivyokuwa wakati ule wa enzi ya benki ya Posta na vitabu vyetu vya benki
Benki Zetu
Mimi bado ninacho kitabu changu cha benki ya Posta, japokuwa sasa hakitumiki lakini nimekiweka kama kumbukumbu za mabadiliko ya benki Tanzania. Nakukumbuka kuchukua kadi yangu ya benki na kuiweka katika mkoba wangu wa ukindu ambao ni bizaa adimu siku hizo, mkoba huu unaitwa kadi, sijui msomaji wa tovuti ya TBC unautambua mkoba huu? maana siku hizi walio wengi wanapenda mikoba ya ngozi na vipima joto tele tele, iwe ya mitumba au special, mie bado nimesalia na mikoba ya ukindu. Maana natambua kikubwa ni kubeba kilicho changu na kuthamini bizaa za nyumbanai Tanzania.

Nipo mkoani Iringa kikazi, hivyo ili niweze kufika mjini, ndipo naweza kupata huduma za kibenki, ni mwendo wa saa kadhaa. Naanza safari yangu kwa mwendo wa saa mbili hivi na ninafika mjini huku tukiambatana na wanakijiji wezangu huku nikipewa salamu nyingi kwa kuwa mimi ni mtumishi wa serikali katika eneo langu ninalofanyia kazi angalau mie ndiye mtumishi wa mfano na kila kona salaam, habari za kazi? hawajambo huko? Ustadhat Nchimbi mzima?

Hayo yakiwa ni maswali ya kawaida na salamu ninazotakiwa kuzijibu, Utumishi wa umma ni mzuri hasa pale unapokuwa mwadilifu. Nilianza safari kwa basi na kutumia saa mbili safarini. Nilifika mjini na ili kuweza kufanya mambo yangu yote ni wajibu wangu kupita benki maana ni Ijumaa ya Januari30 na huku nikiwa na natambua tabia ya benki zetu kuwa na foleni sana hasa kipindi hiki cha mwishoni au mwanzoni mwa mwezi.

Ninahitaji fedha niweze kununua mahitaji ya familia yangu. Nikikaribia benki ya watu wa kipato cha chni nakaribishwa na foleni kubwa ambayo imeanzia ndani hadi nje ya benki. Akilini mwangu nikikumbuka foleni za wakati wa National Milling Corporation na RTC ambapo jambo la kupanga foleni lilikuwa la kawaida ili kuweza kupata mahitaji ya vyakula. Nikiwa benki malalamiko ya wateja hawa ni yale yale mmoja ananiuma sikio kwa kusema “Unapoenda kutoa fedha katika benki yoyote ile unakaribishwa na foleni ndefu. Foleni hizo huwa za aina mbili moja ya kuingia ndani ya benki ambayo inaanzia ndani na ya pili ni kwenye mashine ya kutolea fedha.Huduma inaweza kuendelea kwa kipindi fulani mashine ikiishiwa fedha unajulishwa kuwa mashine ya fedha mbovu”

Anasema mwanamke wa makamo ambaye anaonekana ametokea safari mbali zaidi yangu huku watoto wake wadogo wakimsubiri katika mkululu wa foleni ambayo inaweza kutumia saa sita kumalizika. Hali hii inafanana katika mabenki mengi ambayo yanawateja akina yakhe wateja wa kipato cha chini, huku mabenki hayo yakiwa na kauli mbiu kuwa benki hizo ni za akina yakhe. Pengine wito huo waakina yakhe ni wito unaofanana na adha wanayopata wateja wake kwa kupanga foleni ndefu, huduma kuchelewa, mashine kukorofisha hasa wakati wa mishahara, fikilia mtu ana mgonjwa amelazwa hospitalini,au umekubwa na tatizo lolote lile inakuwaje?

Wengine wakisema benki hizi zipewe jina la benki za watu wa hadhi ya juu nadhani huduma zake zingelingana na hali hiyo lakini kwa akina yakhe yaani sie pangu pakavu tia mchuzi, tabu ni sehemu ya maisha.

Bado nipo benki, ninachungulia ndani ya benki hii la kushangaza kuna madirisha maalumu ya kutoa huduma kwa wateja wenye fedha nyingi na dirisha husika linakuwa halina foleni kabisa huku mhudumu huyo akiwangoja wateja wenye pesa nyingi na kama hilo halitoshi katika mabenki mengine wateja wenye fedha nyingi hupewa huduma katika chumba maalumu kutokana na umuhimu wa uteja wao na usalama wa fedha zao.

Lakini ikumbukwe kuwa wateja wote iwe akina yakhe au wateja wenye hadhi ya juu wao kwa pamoja ndiyo wanaoifanya benki yoyote kuwa na wateja wengi na kipato kingi na kuwa benki kubwa. Suala hili halina ubishi kwani benki zote zimetoka huko katika udogo hadi zimekuwa ni benki kubwa.

Nashangaa kwa muda naamua kwenda kutafuta chumba cha kulala katika chumba cha wegeni angalu nije kupata huduma hiyo usiku, katika mashine ya kutolea fedha, nafika chumba cha wageni na kulala kwa saa kadhaa. Naamka saa mbili na ushehe usiku naelekea katika benki hii ambayo ipo jirani na nyumba ya wageni niliyofikia nakuta mashine haifanyi kazi. Navunjika moyo kabisa, hapa nakutana na wateja wengi wakiwa katika foleni ndefu wakitumaini kuwa mashine hiyo itapona muda si mrefu. Hapa nakutana na kijana mrefu aliyevaa miwani ya giza na sijui kwa muda huo alikuwa akiwezaje kuona.

“Ukubwa wa foleni ni neema kwa watumishi wa mabenki mengi kwani unapokwisha muda wa kufanya kazi na muda zaidi kuanza, hali hii inawapa nafasi watumishi na makarani wa mabenki kupata malipo ya muda wa ziada.” Anasema kijana huyu.

Viongozi wa mabenki wanatakiwa kutambua kuwa ni vizuri mteja kupata huduma kwa haraka ili kumpa nafasi mteja kufanya mambo mengine na wengine kurejea majumbani mwao mapema kufanya shughuli zingine za kimaendeleo kinyume chake benki zetu zitakuwa zinarudisha nyuma maendeleo. Kunakilasababu ya kuboresha huduma zao ili kuwaridhisha wateja wao. Kwa mfano sioni sababu ya kutokuwa na mafundi wa kutosha ili kuweza kuzifanyia mashine zao mara kawa mara ikiwemo kufunga mitambo yenye uwezo na kasi ya mtandao wa mawasiliano Isitoshe ili kuwahudumia wateja vizuri ni vyema wakaweka utaratibu kama wa kudhibiti wateja wanaokologa foleni. Wafanyakazi wa benki na hasa wafundishwe na waelewe vizuri kwamba kila mteja ni mfalme na ana haki sawa na yeyote ili waache utaratibu wa kutoa huduma kwa kujuana.

Huwa nashindwa kujua kama kamera walizozifunga ndani zinawasaidia kusimamia huduma bora. Wamiliki toeni motisha kwa wafanyakazi ili waweze kutuhudumia vizuri. Jambo la msingi kwa mabenki yote na taasisi za fedha zifahamu kuwa huduma za kibenki kwa mteja si hisani bali ni wajibu wao na haki kumpa huduma sitahiki na siyo bora huduma tu Pia taasisi zinazosimamia mabenki haya kuhakikisha mabenki yote yanatoa huduma ya haki kwa wateja wote bila ya kujali uwezo au kiasi cha fedha alichonacho mteja huyo katika akaunti yake Nilisubiri kitambo usiku ule mashine haikupona nilirejea siku ya pili ndipo mashine ikawa inafanya kazi na kupata huduma yangua na kurudi zangu kijijini nilipokuwa natekeleza majukumu yangu. Namalizia kwa kusema dhumuni la kuweka fedha katika benki ni kuhakikisha kunakuwepo utaratibu mzuri wa utunzaji wa fedha na sio kuchimbia fedha chini ya ardhi au kuzificha michagoni. Unapomchelewesha mteja kupata huduma unaweza kuwa ni ujima mambo leo katika huduma za kibenki na ujima mambo leo ni mbaya kuliko ujima wetu wa awali.


Unaweza kuzisikiliza makala hizo hapo chini
Unaweza kusikiliza baadhi ya vipindi hivyo hapa chini.
Msomaji Studioni:   |   Frank Kashonde
Mwandishi:   |   Katherine Nchimbi
Mhariri   |   Adeladius Makwega
Unaweza kusikiliza makala haya hapo chini
MOST POPULAR NEWS