
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Uratibu na Bunge PHILLIP MARMO amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC ina jukumu la kusimamia sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 na ile ya serikali za mitaa ya mwaka 1979 pamoja na marekebisho yote yaliyokwishafanywa wakati wote wa uchaguzi mkuu na uchaguzi mdogo mpaka kipindi kingine cha uchaguzi kinapofika.
Akijibu swali Bungeni Mjini DODOMA Waziri MARMO amesema mtu yeyote atakayevunja sheria hiyo ya uchaguzi anachukuliwa hatua za kisheria na kwamba yapo maeneo mengine ya sheria hiyo yanayohusika na makosa ya jinai ikiwa ni pamoja na jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini - TAKUKURU.
Kuhusua kauli kuwa kuna baadhi ya watu wanaofanya kampeni kabla ya muda kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao, Waziri MARMO amesema iwapo itabainika kuwa watu hao wanavunja sheria itabidi sheria ichukue mkondo wake.
Katika hatua nyingine Bunge limefahamishwa kuwa zaidi ya Watendaji wa Halmashauri Mia Tisa na Ishirini katika Halmashauri Thelathini nchini wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani baada ya kubainika kuwa wamehusika na ubadhilifu wa fedha za umma katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2005/2006 hadi 2009/2010.



