Tanzania Broadcasting Corporation - (TBC)

Thursday
Sep 09th
Text size
  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size
Home

Lukuvi avuruga Ardhi Jiji

WATENDAJI 81 wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam wanaohusika na masuala ya ardhi wamehamishwa na wengine kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Aidha, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, imedaiwa kuwa kinara wa kusababisha dhuluma za ardhi, kutokana na baadhi ya watumishi kuwa na mtandao na watendaji wa Wizara.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, ambaye pia aliwataka wananchi wenye taarifa za kudhulumiwa maeneo ya wazi, kupeleka taarifa kwa wakuu wa wilaya. Lukuvi, ambaye alitangaza hatua zilizochukuliwa dhidi ya maofisa wa ardhi baada ya kupokea taarifa ya tathmini ya kuratibu utawala na upatikanaji wa viwanja kwa Dar es Salaam iliyowasilishwa na kiongozi kamati aliyoiunda, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Sabuni John.

Taarifa hiyo ilibaini kuwa matukio ya dhuluma ya viwanja yamekithiri mkoani Dar es Salaam huku wilaya ya Kinondoni ikiongoza kwa asilimia 90, Ilala asilimia 30 na Temeke asilimia moja. Lukuvi alisema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo na kuporwa maeneo ya wazi, watumishi 40 wanahamishwa kutoka kada mbalimbali ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, 39 wanahamishiwa nje ya mkoa na wawili wanasimamishwa kazi, huku wapiga chapa wakiondolewa na kutafutiwa kazi zingine.

Aliwataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Mkuu wa Kitengo cha Upimaji na Ramani, Hamidu Mgaya ambaye anapisha uchunguzi na John Langasi baada ya kuthibitisha eneo la Msasani kuuzwa. “Huyu Langasi ambaye ni msaidizi wa Magesa (aliyekuwa Ofisa wa Kitengo cha Ardhi Kinondoni), asimamishwe kazi kuanzia leo (jana) na hatua kali za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake, kwani alitoa taarifa ya kuthibitisha uhalali wa eneo la kiwanja Msasani.

Aidha, alisema kuanzia leo idara zote za ardhi katika halmashauri za Jiji zitafanya kazi na kila mwenye barua ya mahali anapotakiwa kwenda afanye hivyo mara moja na wakurugenzi wawapokee na kuwapanga upya. Aliwataka viongozi wote wa Serikali na wanasiasa, wasijihusishe na masuala ya ardhi na kuanzia leo ofisi za ardhi zisiingiliwe na yeyote hata madalali na kama kuna mtu anafuatilia masuala ya ardhi, sharti awe na barua ya kutoka ofisi za kata.

“Kuanzia sasa viwanja vitolewe kwa sheria, viongozi wa siasa, dini waache kushinikiza watendaji ... watendaji waache kupokea maagizo wala taarifa zozote, kwani mwisho wa siku wao ndio watakaoumia,” aliagiza Lukuvi. Alisema baada ya kupokea ripoti hiyo ya ardhi ataikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Polisi na Usalama wa Taifa, kwa kuwa kuna masuala ya uchunguzi ambayo baadaye yanatakiwa kuchukuliwa hatua.

Kuhusu mgogoro wa Kwembe na Kibamba kuhusu fidia ndogo na viwanja vibaya, alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, kwa kuwa Wizara hiyo ndiyo inahusika. “Wananchi wote walioko kwenye maeneo ya wazi waondoke, wakurugenzi andikeni notisi na kama wapo waliojenga wabomolewe na kama wana vielelezo vya usajili wajisalimishe mapema,” alisema Lukuvi.

Rutabanzibwa alisema wizara inahusika kusababisha matatizo yote na kwamba haiwezi kukwepa jukumu la kuchukua hatua, kwa sababu baadhi ya watendaji wa ardhi wa manispaa, madaraka yao yanatoka moja kwa moja wizarani. Hata hivyo, alisema kwa sasa wamepata kasi na nguvu ya kuanza kisayansi zaidi na kushirikiana na halmashauri zote kwa kuwa tatizo ni kubwa.

 
Banner