Tanzania Broadcasting Corporation - (TBC)

Thursday
Sep 09th
Text size
  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size
Home Books Buriani Kawawa, umetangulia

Buriani Kawawa, umetangulia

Buriani Simba wa Vita, ulikuwa mwanasiasa hodari, mtiifu, na jasiri.
Umeufunga mwaka 2009, hukuuona mwaka mpya, kifo chako kimesababisha watanzania tuuanze mwaka mpya wa 2010 kwa majonzi.
Hatutakuona tena Kawawa lakini jina lako litadumu katika historia ya nchi hii. Kawawa hayupo, kaenda, katangulia, ameacha historia yenye furaha na isiyosahaulika.

Hakuna aliyedhani kwamba Februari 27, 2009 alipotimiza umri wa miaka 83 ilikuwa ni mara ya mwisho kwake kusheherekea 'bethidei' yake.
Katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na uzinduzi wa kitabu cha Simba wa Vita katika Historia ya Tanzania, Kawawa alitoa wosia unaostahili kuzingatiwa. Sauti yake ilitoa ujumbe mzito uliodhihirisha kuwa ni wosia wa kuwaonya viongozi kuhusu ubinafsi. Kawawa alisema, ubinafsi wa viongozi ni hatari kwa maslahi ya nchi.

Akasema, katika umri wake wa miaka 83, alikuwa na wajibu wa kuwaasa viongozi wenzake na wananchi kwa ujumla wasitangulize maslahi yao, waweke mbele utaifa. Mzee Kawawa, mtoto wa pili katika familia ya watoto watano ya Zamaladi na Fundi Mfaume Ali,ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 83 na miezi 10. Alizaliwa mwaka 1926 katika Kijiji cha Matepwende, wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Mungu amempenda zaidi mzee wetu ambaye ni miongoni mwa watanzania maarufu si tu kwa umahiri wake katika siasa, bali pia kwa kutungiwa hadithi mbalimbali za utani. Jina lake ni miongoni mwa majina machache yasiyosahaulika kutokana na mchango wake harakati za ukombozi wa Tanganyika na pia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Atakumbukwa kwa kulitumikia taifa kabla na baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake Desemba 9, 1961 aliposhika wadhifa wa Waziri asiye na Wizara Maalumu katika Baraza la Kwanza la Mawaziri chini ya Waziri Mkuu, Mwalimu Julius Nyerere.
Siku 45 baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere alipojiuzulu uwaziri mkuu kwa malengo ya kwenda kuimarisha chama chake cha Tanu, Kawawa alishika hatamu kuongoza nchi katika nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu.

Baada ya Tanganyika kuwa Jamhuri, 1962, Kawawa aliushangaza ulimwengu pale alipoamua kwa hiyari kukabidhi madaraka ya kuongoza nchi kwa Mwalimu Nyerere jambo ambalo katika uwanja wa siasa si rahisi. Utiifu, ujasiri na umahiri wa kiwango cha juu katika kutekeleza uamuzi na malekezo aliyokuwa akipewa, ndiyo yaliyofanya apewe jina la ‘Simba wa Vita’.

Wanaomfahamu Mzee Kawawa, wanamtaja kwamba hakuogopa wala kusita kuchukua hatua katika kutekeleza uamuzi mzito mradi aliamini kwamba kwa kufanya hivyo alikuwa havunji sheria na wala hakiuki kanuni na taratibu za nchi.
Kwa mfano, operesheni ya Ujamaa Vijijini pamoja na maduka ya Ujamaa, Kawawa alikuwa mstari wa mbele kuzitekeleza kwa kutumia muda wake vijijini akihimiza kushiriki kwa vitendo.

Atakumbukwa daima kutokana na mchango wakati katika historia ya vyama vya wafanyakazi. Alihakikisha kwamba siasa inakuwa ni sehemu ya harakati za vyama vya wafanyakazi na hivyo kuundwa kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lililokuwa na nguvu kuliko chama cha wafanyakazi kimoja kimoja.
Mchango wake kwenye vyama vya wafanyakazi, ndiyo uliomwezesha kuingia kwenye Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) kwa malengo ya kuibana serikali ya kikoloni kuvisikiliza na kuvitambua na kuwezsha maslahi ya wafanyakazi.

Mchango wa Kawawa katika kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia ni miongoni mwa mambo ambayo hayawezi kusahaulika. Katika kipindi cha uongozi wake, alijenga na kuimarisha mfumo wa uongozi sanjari na kufanya uamuzi mgumu.
Alijiunga na TANU kwa siri wakati akiwa mtumishi wa Serikali ya Kikoloni katika Idara ya Maendeleo ya Jamii. Mwaka 1958 alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tangu wakati huo hadi sasa, alikuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa. Kawawa aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Tanu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia shughuli za chama, Katibu Mkuu wa CCM wa Kwanza, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM na Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini wa CCM.

Alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa kwanza wa Tanzania,Nyerere kuanzia mwaka 1964 hadi 1972. Baadaye mwaka 1972 hadi 1977 akawa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais. Kwa ujumla, Kawawa akiwa Waziri Mkuu chini ya uongozi wa Nyerere, alifanya mambo mengi. Hata Nyerere aliwahi kumwelezea Kawawa kuwa ni hodari sana, ni kama askari, akipewa kazi huishika kama askari, haogopi kazi wala haogopi matatizo.

Tuzo mbalimbali alizozipata zinadhihirisha umuhimu wake katika taifa hili. Miongoni mwa tuzo hizo ni pamoja na ya Martin Luther, Januari 23, 2007 aliyotunukiwa na Balozi wa Marekani nchini, Michel Retzer ya kutambua mchango wake mkubwa katika harakati za kupigania uhuru wa nchi. Tuzo hiyo ilitolewa pia kutambua mchango mkubwa wa Kawawa katika kulinda na kutetea maslahi ya jamii nchini.

Ukiachia tuzo hizo, pia jamii anayoishi nayo hususan wakazi wa eneo la Kiluvya na Madale katika Manispaa ya Kinondoni alikokwenda kuishi baada ya kustaafu akijishughulisha na ufugaji na kilimo, walikuwa wakimuona Kawawa kuwa ni ni mtu wa watu anayehitaji kuenziwa. Wakazi wa Madale walianza kumuenzi Kawawa hata kabla ya kifo chake kwa kujenga makumbusho yake ikiwa ni njia ya kutambua mchango na ushirikiano wake katika jamii.

“Anaishi kama tunavyoishi, tunashirikiana naye katika masuala mbalimbali. Hata kama anaumwa, akisikia kuna mkutano, atajikongoja mpaka afike mkutanoni,” hii ilikuwa kauli ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Madala, Gration Mbelwa akimwelezea mwanasiasa mkongwe, Rashid Kawawa kabla ya kifo chake.

Bila shaka busara na ushauri wa Mzee Kawawa vingeendelea kuhitajika. Lakini kwa kuwa Mungu amempenda zaidi, mwache atangulie. Maisha yake yataendelee kuwa mfano kwa viongozi wengine nchini. Makaya haya yameandaliwa kwa msaada mkubwa wa kitabu cha Simba wa Vita katika Historia ya Tanzania, Rashid Mfaume Kawawa kilichoandikwa na John M. J. Magotti.
Last Updated ( Tuesday, 23 March 2010 11:36 )  
Banner